ACT: UBABE WA CCM WAINYIMA MAMILIONI WATANZANIA
 
https://rucuso.blogspot.com/2016/03/act-ubabe-wa-ccm-wainyima-mamilioni.html

 TAARIFA KWA UMMA
UAMUZI WA BODI YA WAKURUGENZI YA MCC WA KUSITISHA MAHUSIANO NA TANZANIA YATAWAUMIZA WANANCHI WA VIJIJINI
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeupokea kwa  masikitiko makubwa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa MCC wa kusisitisha  mahusiano na Tanzania.
MCC ni Shirika la misaada la Marekani  lilianzishwa na Bunge la Nchi hiyo mwaka 2004 kwa lengo la kusaidia  miradi ya maendeleo katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya  kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi.
Tangu kuanzishwa kwake, shirika hili  limesaidia miradi mingi ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa barabarani  na usambazaji wa umeme vijijini kwa sasa miradi ya aina hiyo inaendelea  sehemu mbali mbali hapa nchini na miongoni mwao ni pamoja na mradi wa  REA,miradi ya barabara kama ile ya Tnduma Sumbawanga pamoja na Tanga  katika barabara ya Horohoro.
Pamoja na vigezo vingine, kigezo mama  kwa nchi kufuzu kupata misaada ya MCC ni kwa nchi husika kuzingatia  misingi kidemokrasia ikiwemo kufanya uchaguzi ulio huru na haki.
Jana tarehe 28 Machi 2016 Shirika la MCC  lilitangaza kusitisha mahusiano na Tanzania kutokana na serikali ya  Chama cha Mapinduzi (CCM),kubariki kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa  Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba 205 na kubariki kurudiwa kwa  uchaguzi huo tarehe 20 Machi 2016 katika mazingira ambayo hayakuzingatia  misingi ya demokrasia ya vyama vingi na kuvunja matunda ya mwafaka wa  kisiasa na kikatiba uliojengwa kwa gharama kubwa visiwani humo.
Chama cha ACT-Wazalendo kinapigania nchi  yetu kujitegemea kiuchumi kama msingi wa kujenga utu na uhuru endelevu  wa kisiasa na kijamii. Hata hivyo tunatambua kwamba katika kipindi hiki  nchi yetu inahitaji mahusiano mema na Jumuiya ya Kimataifa na wadau  mbalimbali wa maendeleo duniani, likiwemo shirika la MCC, katika  kuendeleza miradi ya maendeleo. Shirika la MCC limekuwa mdau mkubwa  katika miradi ya barabara na kusambaza umeme vijini.
Uamuzi huu wa Bodi ya Wakurugenzi wa MCC utawaumiza na kukwaza juhudi za wananchi wa vijijini katika kujikwamua na umaskini.
Tunasikitika kwamba ubabe wa Serikali ya  CCM na woga wake wa kushindana kidemokrasia umesababisha nchi yetu  ikose pesa za MCC ambazo zingesukuma mbele juhudi za kupambana na  umaskini.
Tunatoa wito tena kwa Serikali ya chama  cha Mapinduzi kuacha ubabe na kufifisha juhudi za miaka ishirini za  ujenzi wa demokrasia hapa nchini. Tunatoa wito maalumu kwa wadau wote wa  siasa visiwani Zanzibar kurudi mezani na kutatua mgogoro wa kisiasa kwa  njia za kistaraabu na katika hali ambayo itarudisha heshima ya nchi  yetu katika kukuza demokrasia nchini.
Imetolewa na
Theopister Kumwenda
Makamu Mwenyekiti, Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje
29/03/2016.