JESHI LA POLISI LAPEWA SIKU 7 TU KUWASILISHA MIKATABA YAKE
 
https://rucuso.blogspot.com/2016/04/jeshi-la-polisi-lapewa-siku-7-tu.html

Na Zuhura Simba
Jeshi la Polisi lapewa siku 7 Liwe Limepeleka Mikataba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za  Serikali (PAC) imelipa siku saba kuanzia jana Jeshi la Polisi nchini  kupeleka mkataba walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi, iliyopewa  zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole kwenye vituo vya  Polisi vya wilaya nchi nzima.
Hadi sasa kampuni hiyo imeshalipwa asilimia 99 ya fedha, ilihali vituo vilivyofunga mashine hizo ni 14 kati ya 108.
Maagizo ya kamati hiyo yaliyotolewa jana  Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilal wakati  kamati hiyo ilipokutana na Jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za  mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za  Serikali (CAG).
Aeshi alisema jeshi hilo mwaka 2011  liliingia mkataba na Kampuni ya Lugumi Enterprises kwa ajili ya kufunga  mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya Polisi vya wilaya  nchi nzima ambavyo viko 108.
Alisema mkataba huo ulikuwa wa Sh  bilioni 37 pamoja na kodi na kwamba hadi sasa kampuni hiyo imeshapewa  asilimia 99 ya fedha zote ili hali vituo vilivyofungwa mashine hizo ni  14 tu, kati ya vituo vyote 108.
“Ukiangalia  kazi iliyofanywa tangu mwaka 2011 hadi leo ni kidogo na pesa hawa  kampuni wameshachukua asilimia 99, sasa tumewaagiza watuletee huo  mkataba ndani ya wiki moja walioingia na kampuni hiyo ili tuupitie,”  alisema Aeshi”.
Kuhusu mali zinazokamatwa na polisi  kwenye matukio mbalimbali nchini yakiwemo ya wizi, Kamati imewaagiza  CAG, Polisi na Mhakiki Mali wa Serikali kufanya ukaguzi wa mali zote  zinazokamatwa na polisi ili kuzifahamu kuzipa thamani halisi kulingana  na idadi yake.
Alisema mpaka sasa mali zinazokamatwa na  polisi hazifanyiwi uhakiki kujua idadi na thamani yake hivyo nyingi  zinapotea bila kujua zilipokwenda na nyingine ambazo kesi zake zimeisha,  zinauzwa kwa bei ndogo kuliko thamani halisi.