JPM, VIMILIA NILALAPO MBELE NA WEWE, HAPA KAZI TU
https://rucuso.blogspot.com/2016/04/jpm-vimilia-nilalapo-mbele-na-wewe-hapa.html
VIONGOZI serikalini wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu, wameombwa na Rais John Magufuli, kuvumilia machungu wakati wa uongozi wake, kama ambavyo wananchi walivyovumilia tangu Uhuru.
Amesema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (flyover) nchini Tanzania, inayojengwa katika makutano ya Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere, eneo la Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan. Machungu hayo kwa mujibu wa Rais Magufuli, yataanza kuonekana wakati wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya kwanza kwa Awamu ya Tano, ambayo fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka asilimia 27 za bajeti iliyopita, hadi kufikia asilimia 40.
Machungu yenyewe Ili kufanikisha dhamira hiyo ya Serikali, Rais Magufuli alisema katika bajeti hiyo inayotarajiwa kupelekwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, litakaloanza vikao vyake Dodoma wiki ijayo, machungu hayo yataanza kuonekana kwani fedha za chai, semina na safari, zimekatwa na kujaziwa katika fedha za maendeleo.
Kutokana na makato hayo, Dk Magufuli amesema kutakuwa na machungu hasa kwa watendaji wa Serikali na kuwaomba mawaziri na makatibu wakuu ambao alisema walikuwa wakifaidi matunda ya Uhuru, wavumilie machungu hayo kwani wananchi wa maisha ya chini wamevumilia machungu kwa muda mrefu.
“Wananchi wamechoka kutuona sisi viongozi tunafaidi matunda ya Uhuru wa nchi tangu Uhuru na wao wakiwa wasindikizaji halafu wao tunawaomba kura na wakishatupigia tunawasahau,” alisema na kuongeza kuwa anataka wananchi watoke kwenye machungu na sasa wawe ‘watamu’ kwa maendeleo.
Magufuli alisema lazima viongozi wabadilike na kurudi kwa wananchi wa maisha ya chini na hiyo itakuwa sadaka kwa kuwapa madaraka kwani wananchi wanyonge wameteseka siku nyingi.
Wasiovumilia Alisema waliokuwa wamezoea chai, safari na posho za ovyo kama wanaona au wanafikiri hawawezi kufanya kazi bila hizo chai, waache kazi mara moja kwani sasa fedha zinazokusanywa za walipa kodi wanyonge, zitaenda kutatua matatizo yao ya hospitali, barabara na kununua ndege za Serikali.