KIZIMBANI KWA KUMUITA MAGUFULI BWEGE FACEBOOK
 
https://rucuso.blogspot.com/2016/04/kizimbani-kwa-kumuita-magufuli-bwege.html
Jeshi  la Polisi Mkoani Arusha, limemkamata Isaack Habakuk Emily, kwa kosa la  kumtukana Rais John Magufuli kuwa ni bwege na kwamba hawezi fananishwa  na Nyerere na kusambaza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza  ofisini kwake, leo jijini Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,  Charles Mkumbo, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 22 mwaka  huu eneo la Hotel ya Anex jijini humo.
Amesema  kuwa baada ya kumkamata alifanyiwa upekuzi na kukutwa na simu ya  kiganjani aina ya Tecno iliyotumika kutenda kosa la kutuma ujumbe wa  kumkashifu Dkt. Magufuli.
Mkumbo  amesema kuwa mtuhumiwa huyo alituma ujumbe wa kashfa kwenye Facebook  usemao:- “Mnamlinganishaje Magufuli na Nyerere,” na kutuma kwa watu  mbalimbali kupitia simu yake ya mkononi.
Mkumbo  amesema mtuhumiwa baada ya kusikia hivyo aliandika tena ujumbe kwenye  mtandao wake usemao, “Hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu  bwege na Nyerere wapi Bwana,” amesema.
Amesema  baada ya kutuma ujumbe huo uliwaudhi watu wengi waliopokea ujumbe huo  na kuwakwaza, hali iliyosababisha kupeleka malalamiko yao Mamlaka ya  Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka hiyo ilitoa taarifa  polisi na hatua za kisheria zilianza kuchukuliwa.
Aidha  amesema baada ya hapo walifanikiwa kumpata mtuhumiwa wa uhalifu kwa  njia ya mtandao, kumtia hatiani na jana alifikishwa mahakamani kujibu  shitaka lake.
Hata  hivyo Jeshi la Polisi limetoa rai wa watu wote kutumia mitandao ya  kijamii vizuri kwa kujiletea maendeleo na kubadilishana taarifa zenye  tija na siyo zenye kuvunja sheria.
Pia amesema Jeshi hilo limejipanga kuwatia nguvuni wale wote watakaovunja sheria kwa kutumia mitandao ya kijamii.




