VPL: SIMBA, YANGA NGOMA DROO 1/10/2016
https://rucuso.blogspot.com/2016/10/vpl-simba-yanga-ngoma-droo-1102016.html
Shiza Ramadhani Kichuya ameifungia Simba bao la kusawazisha katika mechi ya watani wa jadi iliyomalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1 uwanja wa taifa.
Sare ya leo inazidi kuipandisha kileleni Simba SC ikifikisha pointi 17, baada ya kucheza mechi saba, wakati Yanga inatimiza pointi 11 baada ya kucheza mechi sita.
Katika mchezo wa leo Yanga walitangulia kwa bao la Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe kabla ya mzalendo, Shizza Ramadhani Kichuya kuisawazishia Simba SC iliyocheza pungufu kwa muda mrefu baada ya Jonas Mkude kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza.
Goli hilo lilizua tafrani kwa wachezaji wa Simba kumzonga mwamuzi wa mchezo huo Martin Saanya hali iliyopelekea kumuonesha kadi nyekundu nahodha wa Simba Jonas Mkude.
Mashabiki wa Simba walianzisha vurugu kwa kung’oa viti na kuvirusha uwanjani hali iliyopelekea polisi kutumia mabomu ya machozi kuleta utulivu ndani ya uwanja.
Kipindi cha kwanza kikamalizika Yanga wakiwa mbele kwa goli 1-0 huku Simba wakiwa pungufu kufuatia Mkude kuoneshwa kadi nyekundu.
Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa mwamuzi Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
Katika vurugu hizo, Saanya akamtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
Polisi walitumia milipuko kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea.
Kipindi cha pili, Simba SC walibadlika pamoja na kucheza kwa nguvu wakafanikiwa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na winga Shizza Kichuya dakika ya 87 baada ya kona aliyochonga kuingia moja kwa moja nyavuni.