Profesa Lipumba, Lissu wamkataa Muhongo kuteuliwa uwaziri
https://rucuso.blogspot.com/2015/12/profesa-lipumba-lissu-wamkataa-muhongo.html
By Bakari Kiango, Mwananchi
Dar es Salaam. Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu (Chadema) na aliyekuwa mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wamepinga uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Kwa nyakati tofauti, waliliambia gazeti hili jana kuwa msomi huyo hakupaswa kuteuliwa na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo kutokana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow iliyomkuta kipindi alichokuwa akiongoza wizara hiyo.
Pamoja na kupongeza uteuzi wa baraza hilo, walieleza kushtushwa na uteuzi huo wa Prof Muhongo kuingia katika baraza lake la kwanza la Rais Magufuli.
Lissu, ambaye pia ni mwanasheria wa Chadema alisema baraza hilo halina jipya kwani asilimia kubwa ni sura ni zilezile zilizokuwa kwenye Serikali iliyopita.
Alisema Watanzania wasitarajie maendeleo katika baraza hilo kwa sababu miongoni mwa wateule hao walikumbwa na kashfa tofauti.
“Juzi, Rais Magufuli aliifumua uongozi wa Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kashfa, miongoni mwa waziri waliokuwa wakisimamia sekta hiyo ni Dk Harrison Mwakyembe, eti leo (jana), amemrudisha kundini?, “ alihoji.
Aliongeza kuwa kwa mtaji huo kuna haja ya kuanzia harakati alizoanzisha aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kuhusu suala hilo.
“Baraza hili ni kama mvinyo ule ule na chupa ile ile kwa sababu karibu mawaziri wote kamili walikuwa wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete,” alisema Lissu.
Kwa upande wake, Prof Lipumba alisema ameshangazwa na kitendo cha Rais Magufuli kumrejesha profesa mwenzake katika baraza lake hilo na wizara ile aliyopata kashfa ya Escrow iliyomsababisha ajiuzulu.
“Kwa kitendo kama hiki, Rais Magufuli amejiwekea dosari kutokana uteuzi huu. Maana yake ni kuwa katika kashfa ile Prof Muhongo hakuwa na hatia.
Hata hivyo, Prof Lipumba alisema Rais Magufuli ametimiza ahadi yake ya kuunda baraza dogo la mawaziri ili kubana matumizi ya Serikali.
Naye Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Anna Mghwira alisema mchanganyiko huo siyo wa zamani wala mpya katika baraza hilo jipya la mawaziri.
Alisema wote walioteuliwa wanaendana na taswira ya kiongozi wao, hivyo ni mapema kubashiri badala yake Watanzania wasubiri kuona utendaji wao.
“Tangu aingie madarakani Rais (Magufuli) ameonyesha utendaji wake, kikubwa kwa walioteuliwa kuendana na kasi hii ya kiongozi wao,” alisema Mghwira aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi uliopita.
Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha TLP, Macmillan Lyimo alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote badala yake anasubiri Rais Magufuli amalizie kuteua mawaziri wa wizara zilizobaki.
“Tumwache amalize wizara. Huwezi kujua utamu kauacha kwenye wizara hizo zilizobaki,” alisema Lyimo.
Gavana wa kwanza wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Edwin Mtei alimtaka Rais Magufuli kukamilisha mapema uteuzi wa mawaziri kwa wizara zilizosalia.
Mtei ambaye ni mwasisi wa Chadema alimpongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema ana imani mawaziri aliowateua watafanya kazi nzuri ya kupambana na ufisadi.
“Rais ameanza vizuri sasa na hao mawaziri lazima wamsaidie kufanya kazi ya kupambana na wala rushwa, mafisadi na wezi, “alisema.
Hata hivyo, alisema ni muhimu Rais akamaliza mapema uteuzi wa mawaziri wote ili kuepuka watendaji wengine wa Serikali, hasa makatibu wakuu kumhujumu.
“Sijamuelewa anaposema bado hajapata mawaziri wengine, Tanzania kuna watu milioni 45, haiwezekani kukosa nafasi za watu wachache, ila ni kweli lazima wawe waandilifu,” alisema Mtei.